Kiungo Mshambuliaji kutoka Tanzania Simon Msuva amesema bado ni mapema mno kusema kama atarejea Young Africans katika kipindi hiki, licha ya kufanikiwa kushinda kesi dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco.
Simon Msuva anahushishwa na mpango wa kurejea klabuni hapo, huku Simba SC ikitajwa kwenye vita ya kumuwania katika harakati za usajili, kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Akizungumza na Dar24 Media Msuva amesema, amedhamirai kurudi Young Africans katika Maisha yake ya soka, lakini kwa sasa ni vigumu kuthibitisha hilo, kutokana na mipango aliyonayo ya kuendelea kucheza soka nje ya Tanzania.
Amesema anaipenda na kuithamini Young Africans na anatambua mchango wa klabu hiyo katika Maisha yake, lakini hadhani kama muda huu ni sahihi kwake kurejea klabuni hapo.
“Siwakatishi tamaa Young Africans, ipo siku nitarudi kuwatumikia kama ilivyokua kipindi kile, kwa sasa ninafikiria sana kucheza nje ya Tanzania, bado ninatamani kucheza nje, bado nina nguvu ya kucheza nje,”
“Viongozi wengi wa Young Africans nimewahi kukutana nao sana na wamenishawishi sana kujiunga nao, hata viongozi wa Simba SC nao wamekua wakinishawishi, lakini ukweli ni kwamba mipango yangu ni kucheza nje ya nchi.” Amesema Msuva
Msuva aliwahi kuitumikia Young Africans kati ya 2012–2017, kabla ya kutimkia nchini Morocco kujiunga na Difaâ El Jadida aliyoitumikia kati ya mwaka 2017–2020 na kisha alitumkia Wydad Casablanca.
Kati ya Mwaka 2010–2011 Msuva alicheza Azam FC akifunga mabao 11 katika michezo 35 na baadaye alisajiliwa Moro United kati ya mwaka 2011–2012 akifunga mabao 15 katika michezo 37.