Mkurugenzi wa Sheria na Wanachama wa Young Africans, Wakili Msomi Simon Patrick, amebeba jukumu la kumjibu Mchambuzi wa soka kupitia kituo cha Radio cha EFM Jemedari Said Kazumari, kufuatia andiko aliloliweka jana Jumatatu (Agosti 23) kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Jemedari aliweka andiko la kuwataka Viongozi wa Young Africans kusema ukweli kuhusu uharaka wa kuvunja kambi yao nchini Morocco, huku akidai sababu zilizotolewa hazikuwa sahihi.
Madai ya Mchambuzi huyo ambaye amewahi kuwa Afisa Mashindano wa TFF na meneja wa timu ya Azam FC ni kuwa, baadhi ya wachezaji wa Young Africans wamewekwa ‘Karantini’ nchini Morocco baada ya kubainika wana maambuziki ya virusi vya Corona.
Kufuatia madai hayo ya Jemedari, Wakili Msomi Simon Patrick ameandika: “Huwa sipendi kuongelea maoni au mitazamo ya watu binafsi, lakini naomba nijibu hoja za kaka yangu Jemedari Said kama ifuatavyo;
Kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Umma (Public Health Act) ya mwaka 2009, ni marufuku kwa mtu au taasisi kutoa taarifa za ugonjwa au maradhi ya mtu au kikundi cha watu bila idhini ya mamlaka husika, ukifanya hivyo adhabu yake ni faini isiyopungua Laki 5 au kifungo cha miezi 6 au vyote kwa pamoja.
Pia kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu (The Statistics Act), Sheria namba 351 marekebisho ya mwaka 2019, ni marufuku mtu yoyote kutoa takwimu zozote za umma bila idhini ya mamlaka, adhabu yake ni faini Milioni 5 au kifungo kisichopungua miezi 12 au vyote kwa pamoja.
Kwa mujibu wa sheria hizo mbili pamoja na sera ya taifa ya Covid ni marufuku kwa mtu yoyote au taasisi yoyote kutangaza kesi za covid au kutoa takwimu kwa umma bila idhini ya Wizara ya Afya.
Kama kuna wachezaji wamepata Corona basi Klabu imefanya vyema kutotoa taarifa hiyo kwani ni kinyume na sheria za nchi, sio lazima kila kinachofanyika ulaya lazima kifanyike Tanzania ndo kiwe halali, Ronaldo, Zlatan, Aubemayang, Lacazetté wote hawachezi Tanzania, Covid sio suala la FIFA ni la nchi husika.
Ukitaka kuamini maneno yangu, basi kesho kwenye kipindi cha michezo tangazia umma wachezaji unaowajua kuwa na Corona, taja na idadi utafutahi kwa jina la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Klabu imeajiri wataalamu kwenye kila idara ambao huishauri Klabu katika kila jambo. Naomba kuishia hapo, kama kuna hoja itajibiwa kwa hoja.”