Muuguzi mmoja nchini Uingereza anakabiliwa na tuhuma za mauaji ya watoto saba na jaribio la kuwaua wengine 10 katika hospitali ya ‘Countess of Chester’.

Lucy Letby, 32, anakabiliwa na mashtaka 22 ambayo mwendesha mashtaka ameyataja kama ukatili wa mara kwa mara aliyokuwa akifanya katika kitengo cha watoto wachanga cha hospitali hiyo.

Mahakama ilielezwa kuwa mtoaji sumu alikuwa kazini katika hospitali hiyo ambapo visa vya watoto wenye afya wanaokufa vilikuwa vikiongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Kabla ya Januari 2015, takwimu za vifo vya watoto wachanga katika kitengo cha watoto wachanga katika kituo cha Countess of Chester zililinganishwa na vitengo vingine kama hivyo.”

“Hata hivyo, katika muda wa miezi 18 iliyofuata, kulikuwa na ongezeko kubwa la idadi ya watoto waliokuwa wakifariki,” alisema Nick Johnson KC, muendesha mashtaka.

Nick Johnson KC alisema kuongezeka kwa idadi hiyo iligunduliwa na washauri wa hospitali, ambao walipata wasiwasi kwamba watoto wachanga waliokuwa wakifa walidhoofika bila kutarajiwa na ilibainika kwamba vifo hivyo visivyoelezeka vilikuwa na vyanzo vya aina moja.

Johnson alieleza mahakama kwamba kutokana na madaktari kushindwa kutoa maelezo kuhusu vifo hivyo, polisi waliitwa na kufanya uchunguzi wa kina na baadaye ikagundulika kuwa katika kipindi cha kati ya mwaka wa 2015 na katikati ya 2016, mtu mmoja katika kitengo cha watoto wachanga aliwatia sumu watoto wawili.

Inaripotikiwa kuwa Lucy Leby alikuwa zamu wakati watoto wote wawili walipopewa sumu na anashukiwa kuwa yeye ndiye aliyeweka sumu hiyo.

Johnson anasisitiza kuwa vifo hivyo havikuwa ajali na wala sio vya asili na matukio mengi yalitokea wakati wa zamu za usiku.

Hata hivyo, Letby amekanusha mashtaka hayo katika mahakama ya Crown ya Manchester.

Kim afurahia kukamilisha shamba la mboga
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Octoba 11, 2022