Uongozi wa Singida Big Stars umekanusha taarifa za kuachana na Beki wao kutoka nchini Ivory Coastl Pascal Serge Wawa.
Mwanzoni mwa juma hili taarifa zilienea kuwa, Beki huyo ambaye amewahi kuzitumikia Azam FC na Simba SC ameachwa na Klabu hiyo ya mjini Singida katika kipindi hiki cha Dirisha Dogo la Usajili, ambacho kitafikia tamati keshokutwa Jumapili (Januari 15).
Mmoja wa Maafisa wa Singida Big Stars ambaye hakutaka jina lake kuwekwa hadharani amesema, wawa bado hupo klabuni hapo, na kitendo cha kutokuwepo kwenye Michuano ya Kombe la Mapinduzi ulikuwa mpango wa klabu hiyo.
Afisa huyo amesema kuwa, Wawa alipewa ruhusa ya kurejea kwao kwa ajili ya kwenda kumuuguza mzazi wake na atarejea nchini kabla ya mchezo wao dhidi ya Azam FC utakaochezwa Januari 23, Uwanja wa Liti mjini Singida.
“Hizo ni tetesi zinazomuhusu Wawa, kwani hazina ukweli wowote na taarifa rasmi kuhusu timu tunazitoa kupitia viongozi na kurasa zetu za mitandao ya kijamii.”
“Wawa yupo mapumziko, anamuuguza mzazi wake na atajiunga ma timu kabla ya mchezo wetu dhidi ya Azam FC.” amesema kiongozi huyo wa Singida Bisg Stars
Wawa alisajiliwa Singida Big Stars, siku chache baada ya kuondoka Simba SC mwishoni mwa msimu uliopita, na amekuwa chaguo la kwanza la Kocha Hans Van der Pluijm.