Klabu ya Singida Big Stars imetamba kuondoka na alama tatu za mchezo wa Mzunguuko wa 24 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, utakaopigwa keshokutwa Jumatatu (Februari 27), Uwanja wa Liti mkoani Singida.

Singida Big Stars inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza msimu huu 2022/23, imekua na matokeo mazuri kutokana na kuwa na wachezaji wenye uwezo wa kupamabana wakati wote.

Afisa Habari wa Singida Big Stars Hussein Masanza amesema kikosi chao kipo katika maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo, ambao amesema una umuhimu mkubwa sana kwao, kwa sababu wanazihitaji alama tatu.

Masanza amesema wanaifahamu vizuri Mtibwa Sugar, na wanaipa heshima zote kutokana na uzoefu wao katika Ligi Kuu, lakini hilo halitaizuia timu yao kuondoka na alama tatu muhimu keshokutwa Jumatatu.

“Tunajiandaa vizuri dhidi ya wapinzani wetu tunaotarajia kucheza nao siku mbili zijazo, tunafahamu uwezo wao vizuri, hivyo inatufanya pia kujipanga vyema, mpaka sasa timu inafanya mazoezi ya kutosha, tunahitaji alama tatu nyumbani.”

“Tunatambua Mtibwa Sugar ni timu yenye uzoefu mkubwa katika ligi yetu, tunawaheshimu kwa hilo kwa sababu wenzetu wapo kwenye ligi hii kwa muda mrefu sana, lakini hilo halitupi wasiwasi kwa sababu tuna kikosi imara ambacho kinaweza kupata matokeo mazuri dhidi yao.” amesema Masanza

Singida Big Stars inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikifikisha alama 44 sawa na Azam FC iliyo nafasi ya tatu, huku Mtibwa Sugar ikiwa nafasi ya tisa kwa kumiliki alama 29.

Mtibwa Sugar yatamba kushinda ugenini
Mayele: Real Bamako wanatupeleka Robo Fainali