Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddin Nabi amesema kikosi chake kipo salama mjini Bamako, na kimejiandaa kupambana ili kupata matokeo chanya, yatakayokuwa na faida.

Young Africans kesho Jumapili (Februari 26) itacheza dhidi ya AS Real Bamako katika Uwanja wa Machi 26 mjini Bamako, kwenye mchezo wa Kundi C, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Kocha Nabi amesema baada ya kikosi chake kuwasili salama mjini humo, kilianza mazoezi tangu jana Ijumaa (Februari 24), na kimejipanga kucheza kwa ushindani dhidi ya wenyeji.

Amesema lengo kuu la Young Africans ni kuhakikisha mazuri yaliyotokea kwenye mchezo uliopita dhidi ya TP Mazembe yanaendelezwa, ili kujiweka katika mazingira yatakayosaidia kufikia lengo lao msimu huu.

“Tumefika salama na tayari kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo wetu dhidi ya AS Real Bamako, tunafahamu huu ni mchezo mgumu na tumejipanga vizuri kwa mapambano.”

“Hii ni katika kuhakikisha tunaepuka changamoto zozote ambazo zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya majira, hivyo kwa kuwa mchezo wetu utachezwa kesho Jumapili, tutahakikisha kila kitu kinakaa sawa.” amesema Nabi

Baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya TP Mazembe jijini Dar es salaam, Young Africans inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika ikitanguliwa na US Monastir ya Tunisia yenye alama nne.

TP Mazembe ipo nafasi ya tatu kwa kuwa na alama tatu, huku AS Real Bamako iliyoambulia matokeo ya sare ya 1-1 nyumbani mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya US Monastir ikiburuza mkia wa Kundi hilo kwa kuwa na alama moja.

Mayele: Real Bamako wanatupeleka Robo Fainali
TCRA yajadili maboresho uwasilishaji maudhui