Rais, Dkt. John Magufuli ameweka bayana jinsi alivyotatua tatizo la mgao wa umeme ambalo lilisababishwa na kundi la watu kwa maslahi yao binafsi kuamua kukausha maji katika bwawa la kuzalisha umeme Mtera.
Amebainisha hilo leo, Juni 29 alipokuwa anaongea na wananchi Kilosa baada ya kiweka jiwe la msingi ujenzi wa mahandaki katika mradi wa reli ya kisasa SGR.
“Mnakumbuka miaka yote tulikuwa na mgao wa umeme, Mtera maji yamekauka, inanyesha mvua ndani ya wiki moja, kima cha maji kimeshuka chini kumbe palikuwa na watu pale wanakwenda kufungua maji, wanayaachia ili kusudi pawepo na mgao na jenereta ziuzwe” Amesema Rais Magufuli.
Na kuongeza ” Tuliwafukuza wote, leo mtera haija punguka maji, miaka karibu na mitano hamjapata mgao wa umeme, ukikatika kidogo tu unarudi”.
Aidha amesema baada ya kuziba mwanya huo Serikali imeweza kusambaza umeme vijijini kwa bei nafuu 27,000/= tu na vijiji vingi vina umeme sasa na viwanda vinanufaika.