Imefahamika kuwa Mshambuliaji Harry Kane alipigwa marufuku kuingia kwenye uwanja wa mazoezi wa Tottenham hadi atakapokamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Bayern Munich uliogharimu Pauni 100 milioni.
Mshambuliaji huyo alihamia Ujerumani ikidaiwa kwamba ndio usajili uliotikisa katika dirisha la usajili la kiangazi mwaka huu baada ya kudumu Spurs kwa muda wa miaka 20.
Ilikuwa wazi Kane kuwa angeondoka Spurs licha ya mwenyekiti wa klabu Daniel Levy kuweka kiwingu uhamisho huo.
Na wakati akisubiri uhamisho wake kukamilika, inasemekana Kane hakutakiwa kurejea mazoezini kabla ya kukamilisha uhamisho wake wa kwenda Munich.
Hiyo ilimaanisha kwamba mfungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo hakupata nafasi ya kuwaaga wafanyakazi na wachezaji wenzake badala yake alilazimika kusubiri.
Hatua hiyo inaonekana kupingana na msimamo wa Spurs kwamba Mshambuliaji huyo anakaribishwa kurejea katika klabu hiyo wakati wowote licha ya kuondoka.
Kane aliendelea kuwa bize na majukumu yake Tottenham licha ya mazungumzo kuendelea kuhusu uhamisho wake.