Wakala wa beki na nahodha wa kikosi cha Arsenal Laurent Koscielny, amesema mchezaji wake alikua tayari kuondoka klabuni hapo, baada ya kusikia aliyekua meneja wa The Gunners Arsene Wenger ataondoka mwishoni mwa msimu uliopita.
Stephane Courbis wakala wa beki huyo, amesema mipango hiyo ilikua imesukwa na Koscielny kabla ya kupata majeraha ya kisigino alipokua kwenye mchezo wa nusu fainali wa Europa League dhidi ya Atletico Madrid.
Amesema hali hiyo ilikwamisha baadhi ya mipango iliyokua imepangwa na Koscielny kutokana na majeraha ambayo yanaendelea kumuweka nje hadi mwezi Disemba mwaka huu.
“Kwa wakati huo aliamini kila kitu kingewezekana, lakini kuumia kwake na kuwasili mapema kwa meneja mpya wa Arsenal, kulisitisha harakati hizo,” Amesema wakala huyo alipohojiwa na France Football per ESPN.
“Koscielny aliamini asingeweza kucheza soka chini ya utawaa wa meneja mpya, tofauti na Arsene aliyekua amemzoea, lakini aliposikia jina la Unai Emery alifarijika kwa kuona mawazo yake hayakua sahihi,”
“Tayari tulikua tumeshaanza kupata uhakika wa kuondoka jijini London, kufuatia muitukio wa klabu kadhaa za China Na Ufaransa,” aliongeza wakala huyo.
” Koscielny aliniambia asingeweza kusajiliwa na klabu nyingine ya England, kwani alihisi angefanya hivyo alikua anaisaliti klabu ya Arsenal ambayo amedai anaipenda.”
Wakati wakala akifuchua siri hiyo iliyokua imejificha kwa miezi minne, tayari meneja wa Arsenal Unai Emery ameshamthibitisha beki huyo kuwa nahodha wa kikosi chake, licha ya kuwa majeruhi, kwa kuamini anapaswa kuendelea na jukumu hilo.
Mkataba wa Koscielny unatarajia kufikia kikomo mwaka 2020, na anatarajiwa kuanza kucheza soka chini ya utawala wa meneja huyo kutoka nchini Hispania mwezi Januari mwaka 2019.
Koscielny alisajiliwa na Arsenal mwaka 2010 akitokea nchini kwao Ufaransa kwenye klabu ya Lorient-Bretagne Sud, na tayari ameshaitumikia The Gunners katika michezo 238 na kufunga mabao 19.