Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amewaahidi wadau wa usafirishaji ikiwemo madereva na wamiliki wa mabasi kwenda kuongea na Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, ili kuona uwezekano wa baadhi ya mabasi yaendayo mkoani kuondoka saa 11 alfajiri katika stendi ya Magufuli baada ya saa 12 alfajiri.
Ameeleza hayo leo Juni 28, 2021 baada ya kupokea kero kutoka kwa wadau hao wakati wa kikao kilichofanyika bwalo la Polisi Masaki, mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza mbele ya IGP Sirro, mkaguzi mkuu wa kikosi cha usalama wa barabarani wa stendi ya mabasi ya Magufuli, Inspekta Ibrahim Samwix amesema hakuna tatizo lolote kwa mabasi kuondoka saa 11 alfajiri endapo watapata kibali kutaka kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Aridhini (LATRA).
“Afande IGP hakuna tatizo lolote kwa mabasi kuondoka saa 11 alfajiri…, tatizo sio sisi bali ni LATRA ambao hawajatoa ratiba kwa sababu wanasema ofisi ya Waziri ilizuia mabasi kutembea saa 24 kutokana na hofu ya usalama,” amesema Inspekta Samwix.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Madereva wa Mabasi ya mikoani, Abdallah Lubala amesema kitendo cha mabasi 150 kutoka saa 12 asubuhi kwa wakati mmoja ndio chanzo cha mabasi kufukuzana njiani kwa ajili ya kuwahi abiria kwenye vituo vya mikoa na wilaya nyingine.