Mbunge wa Jimbo la Mtama kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amewatahadharisha baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijadiri kuhusu kipande cha sauti ambacho kimekuwa kikisambaa mitandaoni kikihusisha mazungumzo yake na baadhi ya viongozi waandamizi.

Nape amesema kuwa watu hao ni bora wajitathmini kabla hawajaanza kuzungumza kwani suala hilo lina Ujinai ndani yake hivyo waangalie ili wasije kuwa sehemu ya ushahidi.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na Azam Tv, ambapo amesema suala hilo tayari lipo katika vyombo husika likifanyiwa uchunguzi hivyo si vyema kuendelea kulijadiri.

”Hawa wanaojadiri kilichotokea inabidi wawe makini sana, maana suala hili lina ujinai ndani yake na tayari liko katika vyombo husika linafanyiwa uchunguzi, siwatishi lakini uhalisia ndio huo, wajitazame ili wasije kuwa sehemu ya ushahidi,”amesema Nape

Aidha, alipoulizwa kuhusu ukweli wa mazungumzo hayo, Nape amesema si vyema kuendelea kuliongelea suala hilo kwasababu tayari liko kwenye uchunguzi, na vyombo husika vinaendelea kulifanyia kazi.

Hata hivyo, siku za hivi karibuni kuna kipande cha sauti ambacho kilisemekana kuwa ni mazungumzo ya Nape na katibu mkuu mstaafu wa CCM, Abdlrahman Kinana pamoja na William Ngeleja ambapo walikuwa wakijadiri masuala mbalimbali kuhusu kinachoendelea ndani ya chama cha mapinduzi (CCM).

 

JPM amtumbua Makamba, Simbachawene, Bashe waula
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 21, 2019