Mshambuliaji kinara wa mabao katika kikosi cha Mbeya City Sixtus Sabilo amesema baada ya kuhaha kwa muda mrefu na matokeo yasiyoridhisha, ameahidi shughuli rasmi inaanza dhidi ya Simba SC.
Mbeya City itakua mgeni wa mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, keshokutwa Jumatano (Januari 18), mishale ya saa moja usiku.
Sabilo amesema katika mchezo huo watahakikisha wanapambana ili kupata alama tatu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, na anaamini hilo linawezekana kutokana na maandalizi walioyafanya katika kipindi cha majuma mawili.
“Ni muda mrefu hatujafanya vizuri katika michezo yetu, ninaamini katika kipindi cha mapumziko tumefanya maandalizi makubwa na mazuri kwa ajili ya kushinda mchezo wetu unaofuata dhidi ya Simba SC,”
“Sisi Wachezaji tunajua umuhimu wa mchezo huo, tumejipanga kuhakikisha tunazipata alama tatu za mchezo wetu unaofuata, tunakiri Simba SC ina kikosi kizuri lakini hata sisi tuna kikosi kizuri ambacho kinaweza kupata matokeo chanya.” amesema Sabilo
Mchezo wa Duru la Kwanza uliozikutanisha timu hizo, ulishuhudia Mbeya City ikisawazisha dakika za mwisho, na kupelekea kugawana alama, katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mchezo wa Mzunguuko wa 19, Mbeya City ilishindwa kuwika jijini Dar es salaam, kwa kukubali kufungwa 6-1 dhidi ya Azam FC, huku Simba SC ikiichapa Tanzania Prisons 7-1, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini humo.