Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Mazao ya Kilimo cha Songea Namtumbo (SONAMCU), Juma Mwanga amemueleza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa chama chao kimeongeza hamasa kwa vyama vya msingi ili wakulima walime tumbaku na waweze kukidhi mahitaji ya soko.
Mwanga ameyasema hayo wakati Waziri Mkuu akizungumza na wadau wa zao la tumbaku wilayani Namtumbo kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya Nasuli, Ruvuma yaliyowajumuisha wakulima, wanunuzi, wenye viwanda, maafisa kilimo, wasambazaji mbolea na wenye mabenki.
Amesema, “Chama kimeongeza hamasa kwa vyama vya msingi, tulikuwa na wanachama 46 pekee lakini katika msimu wa 2022/2023 tumehamasisha vyama vya msingi vipatavyo 62 na vyote vimeahidi kulima zao la tumbaku.”
Aidha, Meneja huyo pia alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ruzuku ya mbolea ili kumpunguzia mzigo mkulima na kusema, “Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa ruzuku ya mbolea kwani bei ya mfuko mmoja ni sh. 70,000 ukienda popote pale hapa wilayani.”
Hata hivyo, ameiomba Serikali ifanye jitihada za kuajiri maafisa ugani kwenye halmashauri, ili waweze kuwasaidia wakulima wa vijijini na kuhakikisha wanapata mikataba (bilateral agreements), baina yake na nchi za Tunisia, Misri na Algeria ambako kuna wanunuzi wakubwa wa tumbaku ya moshi, inayozalishwa Wilayani humo.