Baada ya Mbunge wa Viti Maalum CCM, Sophia Simba kufukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi na kusababisha pengo Bungeni, Kamati Kuu ya CCM (NEC) imemteua Dkt. Getrude Rwakatare kuwa mbunge wa viti maalum na kuziba pengo hilo.
Aidha, taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari imesema kuwa uteuzi wa Rwakatare umefanyika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 kifungu cha 86A(8) cha sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 348.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi, Ramadhan Kailima amesema kuwa uteuzi huo umefuata taratibu za kisheria.
“Baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Spika Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, kifungu cha 37(3) cha sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura 343 Spika wa Bunge aliitarifu NEC kuwepo kwa nafasi ya iliyopo wazi ya mbunge wa viti maalum kupitia CCM baada ya aliyekuwa mbunge, Sophia Simba kuvuliwa uanachama,”amesema Kailima
Hata hivyo, Sophia Simba aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake CCM (UWT) Taifa alifukuzwa uanachama kwa kosa la maadili kinyume cha kanuni za uongozi alilofanya wakati wa Uchaguzi mwaka juzi pia walikuwepo wanachama wengine 11 waliofukuzwa uanachama wa chama hicho.