Baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameungana na Ofisi ya Rais TAMISEMI  pamoja na vikundi vya Jogging Mkoani Dodoma kufanya mazoezi kuunga mkono agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan la kufanya mazoezi.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo  Afisa Tawala kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Rose Lugendo amewaomba wakazi wa Dodoma wajitokeze kwa wingi kufanya mazoezi kwa afya zao na kuimarisha mahusiano baina yao.

“Napenda kuwashauri wakazi wa Dodoma kujiunga na Jogging Clubs na kuwa na Utamaduni wa kufanya mazoezi kwa Afya zao,” amesema Lugendo.

Kwa upande wake Mbunge Wa Mtera, Livingstone Lusinde amewaasa vijana kujitokeza kufanya mazoezi kila siku na sio kusubiri kufanya mazoezi mara moja kwa mwezi kwasababu mazoezi ni sehemu ya maisha.

Naye Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago amevipongeza vikundi vya Jogging Dodoma kwa kuleta mwamko wa mazoezi katika mkoa wao na kujenga desturi ya watu kupenda mazoezi na michezo.

Hata hivyo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Dodoma Mjini, Daniel Shija amewahakikishia ulinzi wanamazoezi na michezo kwa ujumla katika sehemu mbalimbali ambazo watakuwa wanafanya michezo.

Jeshi la Polisi latangaza vita isiyo na kikomo dhidi ya wahalifu
Sophia Simba apata mrithi viti maalum CCM