Hatimaye rungu la Chama Cha Mapinduzi limewashukia wale waliokutwa na hatia ya kukisaliti chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, huku Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba aking’olewa rasmi ndani ya chama hicho.
Taarifa kutoka ndani ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) zimeeleza kuwa Sophia Simba amevuliwa rasmi uanachama wa chama hicho, hatua ambayo inamfanya kuvuliwa pia ubunge wa viti maalum kupitia chama hicho.
Hivi karibuni, Sophia Simba alitangaza kutogombea tena nafasi ya Uenyekiti wa UWT baada ya kuiongoza jumuiya hiyo kwa miaka mingi.
Wengine waliotiwa hatiani ni Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye sasa ni Balozi, Josephine Genzabuke (Mbunge) na Adam Kimbisa (Mwenyekiti wa CCM-Dodoma) ambao wamepewa onyo kali kwa njia ya maandishi.
Uamuzi huo umefikiwa leo baada ya kukamilika kwa vikao Kamati za Maadili na Kamati ya Kuu ya chama hicho mjini Dodoma, na kisha uamuzi kutangazwa katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa, chini ya mwenyekiti wa chama hicho tawala, Dkt. John Magufuli.
Julai 10 mwaka juzi, Dkt. Nchimbi na wajumbe wenzake wawili wa Kamati Kuu, Sophia Simba na Adam Kimbisa walitoka hadharani wakisema wazi kuwa hawakubaliani na uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho kuyaondoa majina ya wagombea likiwemo jina la Lowassa wakidai utaratibu uliotumika ulikiuka katiba.
Dkt. Magufuli alitangaza kuwashughulikia na kuwachukulia hatua kali wale wote waliokisaliti chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita, muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo dhidi ya aliyekuwa mpinzani wake mkuu, Edward Lowassa aliyekihama chama hicho na kutimkia Chadema ambapo alipewa nafasi ya kugombea.