Kocha mkuu wa timu ya taifa ya England Gareth Southgate ametangaza kikosi kitakachoingia kambini mwishoni mwa juma lijalo, tayari kwa maandalizi ya mchezo wa kuwania kufuzu fainali za UEFA Nations League dhidi ya Hispania.
Southgate ameendelea kuifanyia kazi sera ya kuwaita vijana katika kikosi cha nchi hiyo, kama alivyofanya wakati wa fainali za kombe la dunia zilizofanyika nchini Urusi, na England kufika hatua ya nusu fainali na baadae kushika nafasi ya nne.
Beki wa kushoto wa Man Utd Luke Shaw ni miongoni mwa walioitwa na kocha huyo, huku Ashley Young, ambaye alicheza michezo sita ya fainali za kombe la dunia akiachwa.
Southgate pia amemuita mshambuliaji wa majogoo wa jiji Liverpool Adam Lallana, James Tarkowski wa klabu ya Burnley na Alex McCarthy kutoka Southampton.
Jamie Vardy pamoja na Gary Cahill ambao mapema juma hili walitangaza kujiweka pembeni na timu ya taifa ya England, nao wametajwa katika orodha ya wachezaji ambao huenda wakajumuishwa, endapo dharura yoyote itajitokeza katika maandalizi ya mchezo dhidi ya Hispania.
England watakua wenyeji wa Hispania Septemba 08 kwenye uwanja wa Wembley, ikiwa ni mwanzo wa kusaka safari ya ushiriki wa michuano ya UEFA Nations League.
Baada ya mchezo huo, The Three Lions watacheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Usiwz siku tatu baadae kwenye uwanja wa klabu ya Leicester City (King Power Stadium).
Kikosi kamili kilichotajwa na kocha Southgate upande wa makipa yupo Jack Butland (Stoke), Jordan Pickford (Everton) na Alex McCarthy (Southampton).
MABEKI: Trent Alexander-Arnold (Liverpool), Fabian Delph (Manchester City), Joe Gomez (Liverpool), Harry Maguire (Leicester City) Danny Rose (Tottenham Hotspur), Luke Shaw (Manchester United), John Stones (Manchester City), James Tarkowski (Burnley), Kieran Trippier (Tottenham Hotspur) na Kyle Walker (Manchester City)
VIUNGO: Dele Alli (Tottenham Hotspur), Eric Dier (Tottenham Hotspur), Jordan Henderson (Liverpool), Adam Lallana (Liverpool), Jesse Lingard (Manchester United) na Ruben Loftus-Cheek (Chelsea).
WASHAMBULIAJI: Harry Kane (Tottenham Hotspur), Marcus Rashford (Manchester United), Raheem Sterling (Manchester City), Danny Welbeck (Arsenal).