Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya England, Gareth Southgate amesema endapo taifa hilo litapata mafanikio kwenye Fainali za Mataifa ya Bara la Ulaya ‘EURO 2024’ ataongeza mkataba mwingine na Uongozi wa Chama cha Soka ‘FA’.
Southgate aliteuliwa kuwa Kocha Mkuu timu ya Taifa ya England baada ya Sam Allardyce kuachia ngazi mwaka 2016.
Kocha huyo ameiongoza England kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi na kumaliza nafasi ya tatu kwenye michuano ya UEFA Nations League.
England ilikabiria kubeba ubingwa wa EURO mwaka 2020 kwenye fainali iliyochezwa katika Uwanja wa Wembley dhidi ya Italia, aidha Southgate akakiri uwepo wake ndani ya kikosi hicho itategemea mafanikio watakayopata kwenye michuano hiyo ambayo itafanyika mwaka 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari, Southgate ameweka wazi hatima yake kuelekea mechi zao za kufuzu michuano hiyo.
“Itategemea kama tutafanikiwa kwenye michuano hii (EURO), nadhani unatakiwa uwe makini kwa kila kitu ambacho unafanya, mafanikio yanatokea kutokana na kikosi chako, ukiwa na wachezaji fiti na uwezo kila kitu kinawezekana,” amesema Southgate Alipouliza kama atainoa England endapo watafanikiwa kubeba ubingwa wa michuano hiyo Southgate akajibu: “Maamuzi yatafanyika muda muafaka ukifika,” ameijibu kauli hiyo huku akicheka.