Kampuni ya kubashiri ya SportPesa imetoa taarifa ya kusikitishwa sana na uamuzi uliochukuliwa na uongozi wa Young Africans SC wa kukiuka makubaliano yao ya kimkataba na kuzindua jezi mpya zenye jina la mfadhili mwingine.
Kupitia taarifa kwa umma, SportPesa imewafahamisha wateja wake na umma kwamba bado ni Mdhamini Mkuu wa Klabu na ina haki ya kipekee ya kuwa kifuani mwa Young Africans kwa miaka mitatu (2022-2025).
Ombi la Young Africans kupata mdhamini mwingine kwa ajili ya hatua inayofuata ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, lilikuwa ni kukiuka makubaliano yake na klabu hiyo na lilikatisha tamaa sana lilipowasilishwa kwao.
“SportPesa inafahamu kikamilifu maagizo na sheria za CAF kuhusu utangazaji/ufadhili uliopo na ilikuwa imetumia kauli mbiu ya “Visit Tanzania” kuchukua nafasi yetu ili kufuata masharti yanayohitajika kutoka kwa CAF.”
“Kampeni hii mbadala ya “Visit Tanzania” ilifanikiwa kuitangaza nchi nzima kwa misimu miwili iliyopita ya CAF, lakini pendekezo letu lilikataliwa kwa kuwa klabu ilikuwa tayari imeamua kuuza haki hizi bila kujali masharti ya kimkataba yaliyopo na SportPesa.”
“SportPesa inahifadhi haki yake ya kuomba fidia na msaada kutoka kwa mamlaka husika kwa uharibifu uliosababishwa.” imeeleza taarifa ya SportPesa kwa umma.
Young Africans juzi Jumatatu (Januari 31) ilisaini mkataba na kampuni ya Haier wenye thamani ya Tsh bilion 1.5 kama mdhamini mkuu wa Kombe la shirikisho Barani Afrika Hatua ya Makundi msimu huu 2022/23.