Umoja wa wachezaji mpira wa miguu Tanzania (SPUTANZA) umewataka wachezaji wanaomaliza mikataba yao, kujitambua na kujithamini katika kipindi hiki cha kuelekea ukingoni mwa msimu wa 2019/20.
SPUTANZA wametoa wito hiyo kufuatia tetesi za usajili kuanza kuchukua nafasi katika klabu kadhaa za soka hapa nchini, licha ya ligi ya msimu huu kusimama kupisha mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya CORONA (COVID 19).
Mwenyekiti wa umoja huo Mussa Kisoki amezungumza na Dar24 na kusema, kipindi hiki wachezaji wanapaswa kujitambua kama wafalme na wasikurupuke kufanya maamuzi kwa sababu ya kutajwa kwenye klabu fulani.
Amesema mchezaji yoyote anapaswa kutambua thamani yake na asibabaishwe na maneno ya vyombo vya habari ama wanachama ambao wamekua chagizo la kutoa ushawishi ili wajiunge na klabu zao kwa gharama za kawaida.
“Wachezaji kwa sasa ni wafalme, wanapaswa kujitambua kikamilifu, huu ndio wakati wao wa kutengeneza maisha na kujiwekea misingi ya heshima kwa yoyote anaemfuata ili aweze kusaini fomu za usajili wa kuelekea msimu ujao wa ligi,”
“Kuna watu wababaishaji wanaweza kutumiwa ili kuwarubuni na kujikuta wanaingizwa mkenge, lakini rai yetu kama SPUTANZA wachezaji wanatakiwa kupevuka na kuachana na kasumba hizo, ambazo hutumiwa kila mwaka ili kuwarubuni na mwisho wa siku wanajiuta wanaingizwa mjini kwa kupewa fedha ambazo hazina thamani sawa na viwango vyao.”
SPUTANZA imekua mstari wa mbele kusimamia haki za wachezaji hasa inapojitokeza hatua ya klabu kushindwa kulipa stahiki za wanachama wake, pindi mkataba unapokwisha ama kuvunjwa, lakini rai hii kutoka kwa kiongozi mkuu inapaswa kupokelewa kwa mashiko.