Harakati za kusaka tiketi ya kushiriki fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) 2022 kwa timu ya taifa ya Tanzania *Taifa Stars* zinaendelea tena leo Jumanne Novemba 17 dhidi ya Tunisia, kwenye Uwanja wa Benjamin Mpaka, Dar es salaam.
Stars itashuka uwanjani ikiwa na kukumbukumbu ya kufungwa bao moja kwa sifuri Ijumaa iliyopita mjini Tunis, hivyo hii leo italazimika kusaka ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri katika msimamo wa kundi J, ambalo Tunisia ipo kileleni ikiwa na alama tisa ikifuatiwa na Equatorial Guinea yenye alama sita baada ya juzi kuichapa tena Libya iliyopo mkiani ikiwa na alama tatu sawa na Tanzania.
Hivyo, Libya na Equatoria Guinea zenyewe zimeshacheza michezo minne, wakati Taifa Stars na Tunisia leo ndio zitakamilisha mzunguuko wanne katika kundi J.
Tayari Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, amesema amefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mechi iliyopita, na anaamini katika kujituma kwa wachezaji ndiyo silaha pekee ya ushindi katika mchezo huo, utakaoanza saa nne kamili usiku.
“Tunisia ni timu kubwa, lakini tutakuwa nyumbani na vijana wangu naamini wataipambania bendera ya taifa, ukibeba bendera ya taifa lazima ujitolee, tumeamua kujitoa hii ni timu ya taifa kila mtu lazima ajitolee,” amesema kocha huyo kutoka nchini Burundi, huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Idara Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo jana alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, ambapo alisema kulingana na mabadiliko ya muda wa mchezo huo, idadi ya mashabiki watakaowaruhusu kuingia kushuhudia ni 20,000 tu.
Alisema idadi hiyo ya mashabiki inatokana na utaratibu uliowekwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), katika kipindi cha hiki cha kupambana na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.
“Mashabiki wanatakiwa kuzingatia sheria na maagizo ya CAF kuhusu utaratibu, ni kukaa umbali kidogo, ninaimani Watanzania watazingatia hilo ili tuweze kupata fursa hiyo kwa klabu zetu za Simba na Namungo ambazo zinaiwakilisha nchini kwenye michuano ya kimataifa,” alisema Singo huku akisisitiza kuhusu usalama kila kitu kipo vizuri.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao, alisema walijaribu kuomba mechi hiyo isichezwe usiku wa saa 4:00, badala yake muda urudishwe nyuma na kuwa saa 1:00 au saa 2:00 usiku, lakini CAF ilikataa.
“Tuliongea CAF walikataa wakitoa sababu kuwa haki ya matangazo ya televisheni inawabana na isingewezekana kwa mechi hiyo kuchezwa saa 1:00 au saa 2:00,” alisema Kidau.
Tunisia inahitaji ushindi ili kufuzu fainali hizo, ambazo kwa Stars kama ikifuzu, itakuwa ni mara ya tatu katika historia ya Tanzania kushiriki michuano hiyo mikubwa zaidi barani Afrika.