Nahodha na Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Mbwana Ally Samatta amesema wamejipanga kupambana na kuanza vyema Kampeni za kuwania tiketi ya kufuzu Fainali za AFCON 2023 zitazounguruma nchini Ivory Coast.
Taifa Stars itaanza Kampeni hiyo kesho Jumamosi (Juni 04), kwa kucheza ugenini dhidi ya Niger nchini Benin, na tayari imewashawasili Cotonou kwa ajili ya mchezo huo, utakaoanza majira ya saa moja kwa saa za Afrika Mashariki.
Samatta amesema dhamira kubwa waliyoondoka nayo jijini Dar es salaam jana Alhamis (Juni 02), ni kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo huo wakiamini kufanya hivyo itawawezesha kuwa na mwanzo mzuri wa safari yao ya kucheza AFCON 2023.
“Mawazo yetu ni kuanza vizuri kampeni za AFCON 2023, kwa sababu ndio mchezo wetu wa kwanza, bahati mbaya tunaanzia ugenini, lakini upande mwingine ni bahati nzuri kwa sababu unapopata matokeo mazuri ugenini kwa kiasi fulani inakuongezea kujiamini katika kamepni nzima, kwa hiyo lengo ni kwenda kuanza vizuri.”
“Tunaamini mipango na mikakati yetu itatimia kwa sababu tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo wetu wa kesho dhidi ya Niger, niwaombe watanzania kuwa kitu kimoja na kuiombea timu yao ili iweze kufanikiwa kupata ushindi kesho na kufanikiwa kupata tiketi ya kucheza AFCON 2023.”
“Tunafahamu Niger nao wanatamani kwenda kushiriki Fainali za AFCON mwakani, sisi pia tunatamani kurudi tena baada ya kushiriki miaka miwili iliyopita, kwa hiyo lazima mchezo utakua mgumu, kwa sababu kila timu inaamini kwamba kuanza vizuri katika mchezo wa kwanza maana yake unapata nafasi ya kuwa na Kampeni nzuri” amesema Samatta.
Baada ya mchezo wa kesho Jumamosi (Juni 04), Stars itarejea jijini Dar es salaam kucheza mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi F dhidi ya Algeria utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Juni 08.