Mvua zinazoendelea kunyesha Jijini Dar es salaam zimesababisha uharibifu na adha kubwa kwa baadhi ya sehemu ambazo miundombinu yake bado haiko vizuri, Watumiaji wa Stendi ya Mabasi ya Mbagala Rangitatu wameiomba Manispaa ya Temeke kuboresha miundombinu ya stendi hiyo katika kipindi hiki ili kuondoa adha wanayokabiliana nayo ya kujaa maji.
Aidha Ombi hilo limetolewa Jijini Dar es Salaam na abiria, wafanyabiashara na madereva wanaotumia stendi hiyo wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto hiyo.
Afidh Abdallah ni mfanyabiashara katika stendi hiyo, amesema kuwa katika kipindi hiki cha mvua stendi hiyo imekuwa ikijaa maji na kusababisha matope hivyo kusababisha adha kwa watumiaji.
“Mvua ikinyesha hatuwezi kufanya biashara katika stendi hii tunashindwa kuzunguka kufuata wateja” amesema Abdallah.
 Kwa upande wake Mama Lishe katika stendi hiyo, Mwajabu Mohamed amesema kuwa maji yanapo jaa katika stendi hiyo wateja wao wamekuwa wakishindwa kufika kupata chakula kutoka maeneo mengine kwa kuhofia madimbwi na matope yanayokuwepo.
Naye, Said Khatibu ambaye ni dereva wa basi ambalo linafanya safari zake kati ya Dar es Salaam na mikoa ya kusini amesema kuwa wakati huu wa mvua changamoto kubwa inayokuwepo eneo hilo ni kushindwa kupata nafasi ya kupakia na kushusha abiria kutokana na maji na tope linalokuwepo.

Spika Ndugai: Nitahakikisha chadema wanapata haki yao EALA
Wananchi watakiwa kuweka kando itikadi zao