Kiungo Mshambuliaji kutoka Burkina Faso Stephen Aziz Ki ameitumia salamu Simba SC, kwa kusisitiza msimu huu watahakikisha Young Africans itatetea Taji la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo.
Young Africans ilitwaa Ubingwa msimu uliopita 2021/22 kwa Rekodi ya kushinda michezo yote 30 ya Ligi Kuu, Rekodi ambayo inaendelea hadi msimu huu 2022/23.
Aziz Ki ambaye alisajiliwa Young Africans mwanzoni mwa msimu huu akitokea kwa Mabingwa wa Ivory Coast ASEC Mimosas, amesema mipango mikubwa klabuni hapo ni kuhakikisha wanaendelea kushinda michezo ya Ligi Kuu, ili wajizatiti kileleni na kulinda heshimaya Ubingwa.
Hata Hivyo Kiungo huyo amekiri kuiheshimu Simba SC katika mbio za Ubingwa msimu huu, kutokana na kuwa na kikosi bora na imara, lakini bado akasisitiza Young Africans ni bora zaidi na ina mipango madhubuti ya kutetea Ubingwa wake.
“Mipango yetu haijabadilika bali ni kuhakikisha tunatetea Ubingwa ambao tuliutwaa msimu uliopita, naheshimu ubora wa wapinzani wetu hususan Simba SC, lakini naamini kwa ari ya wachezaji ninayoiona kwenye mazoezi na mipango thabit ya Uongozi tutafanikisha hilo.” amesema Kiungo huyo aliyefunga bao la kusawazisha kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 17, baada ya kuifunga KMC FC jana Jumatano (Oktoba 26), ikiwa mbele kwa mchezo mmoja dhidi ya Simba SC yenye alama 14.
Simba SC itacheza leo Alhamis (Oktoba 27) na Azam FC Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.