Klabu nguli nchini Hispania FC Barcelona imekubali kumuachia mshambuliaji Luis Alberto Suárez Díaz, ajiunge na wababe wa mjini Madrid, Atletico Madrid ambao wanashiriki Ligi Kuu ya Hispania La Liga.
Suarez anaondoka FC Barcelona, kufuatia kutokua sehemu ya mipango ya meneja mpya wa Barca Ronald Koeman, ambaye amedhamiria kufanya mabadiliko kwenye kikosi cha klabu hiyo ya Camp Nou.
Hata hivyo FC Barcelona walikuwa radhi kumuachia Suarez ambaye ni raia wa Uruguay kujiunga na klabu yoyote bila ada usajili, lakini kwa sharti la klabu hiyo kuwa nje ya Hispania (isiyoshiriki La Liga).
Rais wa FC Barcelona, Josep Maria Bartomeu alizuia uhamisho wa Suarez kwenda Atletico Madrid kwa sababu hakutaka nyota huyo auzwe kwa washindani wao.
Suarez alikuwa tayari kupunguziwa mshahara ili ajiunge na klabu hiyo ya Madrid, baada ya mpango wa kusajiliwa na mabingwa wa Italia FC Juventus kukwama, kufuatia changamoto za kupata uraia na kibali cha kufanyia kazi.
Atletico Madrid wamejinadi kutoa kiasi cha Pauni milioni 5.5 ili kuhitimisha usajili wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 33, huku ikielezwa huenda fedha hizo zikaongezwa kufuatia makubaliano ya pande hizo mbili.