Mapigano kati ya Jeshi la Sudan na kikosi cha akiba cha Rapid Support Forces – RFS yanaendelea katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum baada ya mazungumzo yanayolenga kutafuta suluhu na kupunguza mzozo wa kibinadamu kuvunjika.
Wakazi wa jiji hilo na mji jirani wa Omdurman, wamesema jeshi limefanya mashambulizi ya anga na kutumia mizinga wakati mapambano yakiendelea, bila ya uwepo wa dalili ya kikosi cha RSF kuondoka katika mitaa ya jiji hilo.
Takriban ikiwa ni wiki ya saba tangu kuanza kwa mapigano hayo, hakuna hali ya utulivu katika eneo kubwa, huku watu milioni 12 wakikosa makazi ndani ya Sudan na wengine 400,000 kukimbilia mataifa jirani kuomba hifadhi.
Marekani na Saudi Arabia mwishoni mwa wiki iliyopita zilisitisha mazungumzo ya amani baada ya sitisho la mapigano walilosimamia kuvunjika, na kuzishutumu pande zote mbili kuvamia nyumba, biashara na Hospitali na kufanya mashambulizi ya anga.