Marekani Norway, Uingereza na Umoja wa Ulaya wameionya Sudan juu ya uteuzi wa waziri mkuu mpya baada ya kiongozi wa kiraia Abdallah Hamdok kujiuzulu katikati ya maandamano ya kuupinga utawala wa kijeshi, huku zikisema hatua hiyo inaweza kulitumbukiza taifa hilo kwenye mzozo.
Mataifa hayo kwa pamoja wamesema hawatamuunga mkono Waziri Mkuu atakayeteuliwa, iwapo wadau wengi wa kiraia hawatahusishwa, imesema sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani.
Taarifa hiyo ya pamoja pia imetoa mwito wa kuendelea kwa maandalizi ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka 2023 chini ya makubaliano ya kipindi cha mpito, lakini pia kuimarishwa kwa mfumo wa huru wa mahakama na bunge, huku ikionya hatua ya upande mmoja ya kuteua waziri mkuu mpya na baraza la mawaziri inaweza kudhoofisha uaminifu wa taasisi hizo.
Mataifa hayo manne yenye nguvu kubwa kiuchumi ulimwenguni aidha yamesema bado yanaamini katika mabadilishano ya madaraka kwa njia ya demokrasia nchini Sudan, lakini kwa upande mwingine yakalionya jeshi iwapo litashindwa kuchukua hatua za kusonga mbele.
Waziri mkuu wa zamani, Abdalla Hamdok, alijiuzulu siku ya Jumapili huku kukiwa na mkwamo wa kisiasa na maandamano makubwa yaliyotokana na mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba.