Waziri wa viwanda na biashara, Innocent Bashungwa amesema mzigo wa sukari kutoka nje ya nchi ambayo inaziba pengo la upungufu wa asilimia 20 ya uhaba wa sukari tayari imeingia nchini na imeanza kusambazwa.
Bashingwa amesema hayo leo Aprili 16, 2020 alipokuwa anaongea na waandishi wa habari juu ya taharuki iliyojitokeza baadhi ya maeneo nchini ya kupanda kwa bei ya sukari.
“Tulitoa vibali vya kuingiza sukari miezi michache iliyopita, lakini kuanzia jana tayari ule mzigo wa kwanza wa tani elfu kumi unapakuliwa bandarini na kufikia leo jioni tayri tani elfu tano zitakuwa zimeshaingia mtaani”
Amesema serikali intambua kuwa mwezi wa ramadhani unakaribia, hivyo watanzania wanatakiwa kutokuwa na hofu juu ya upatikanaji wa sukari na bei kupanda kwani hadi mwisho wa mwezi huu, tani elfu 20 zitakuwa zimesambazwa mtaani na mwezi Mei nyingine 20 zitaingizwa.
Changamoto ya usafiri baada ya mlipuko wa janga la corona amesema kwa Tanzania haijawa na athari kubwa kwa usafirishaji wa sukari kwani walianza mipango muda mrefu kabla ya ugonjwa huo.
Bashungwa amesema uzalishaji wa sukari kwa viwanda vya ndani umepungua kwasababu ya msimu ya mvua, miwa inaathirika haitoi sukari nyingi lakini kipindi cha mvua kitakapo kwisha uzalishaji utaongezeka.
Aidha ametoa tahadhari kwa wafadhabishara ambao wameficha sukari kutoa kwani kuna jopo la wakaguzi limetumwa kukagua kwani mwezi wa ramadhani umekaribia na wananchi wanatakiwa kupata sukari kwa wingi.