Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais wa Young Africans Suma Mwaitenda amefungua rasmi kampeni zake leo Jumatano (Julai 06), Makao Makuu ya Klabu hiyo jijini Dar es salaam.
Mwaitenda amejitosa kuwania nafasi hiyo, ikiwa ni mara yake ya pili kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu wa Young Africans, akifanya hivyo miaka minne iliyopita kwa kugombea nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
Mwanachama huyo wa Young Africans amesema amedhamiria kuingia kwenye uchaguzi kwa utashi wake kama Mdau wa Soka kupitia Young Africans, wala asichukuliwe anatumia nafasi yake kama Mwanamke.
Amesema anaamini anatosha katika nafasi ya Makamu wa Rais wa klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Masharki na Kati, kwani anaifahamu vizuri, na endapo atapata nafasi atahakikisha anafanya kazi kwa kumsaidia Rais atakayechaguliwa Jumamosi (Julai 09).
“Mimi siombi kura kwa sababu mimi ni Mwanamke. Mimi nawaomba Wanachama wapime uwezo na uzoefu wangu na sio ishu ya Jinsia”. Amesem Suma Mwaitenda
Katika hatua nyingine Suma Mwaitenda ameonesha kukerwa na kitendo cha Mgombea Urais wa klabu hiyo Engineer Hersi Said kuchagua upande mmoja wa mpinzan wake Arafat Haji.
Wawili hao jana walizindua kampeni zao kwa pamoja katika mkutano na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam, hali ambayo imeleta sura ya kubebana mapema kwa ajili ya kuingia madarakani.
“Siwezi kumukuhumu mgombea kumchagua Mgombea mwingine, japokua kimkakati inaweza isiwe sawa kufanya vile, kwa mtazamo wangu, kwa sababu wote ni Wagombea, “
“Yanga sio ushiriki wa Wagombea Wenza kama Vyama vya Siasa, kama umeamua kugombea unatakiwa kujipambanua kwa kueleza sera zako, una lengo gani, una hoja gani na unataka kufanya nini?”
“Hakuna mtu atakayefanya kazi mwenyewe baada ya kuchaguliwa, lakini bado haiondowi kila mmoja kunadi sera zake kwa kubebwa na mwingine, mimi ninawatakia heri, ninafanya kampeni zangu, na Wanachama wanapaswa kuchagua kwa kuangalia nani anafaa kuwavusha kwenda kwenye Nchi ya Ahadi.” Amesema Suma Mwaitenda