Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ametangaza kurudi Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiwa ni takribani miezi miwili tangu ajitoe ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Sumaye ametangaza uamuzi huo leo, Februari 10, 2020 na kupokelewa na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally katika Ofisi ndogo za chama hicho zilizoko mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mbele ya wanachama wa chama hicho waliofika kumpokea akiwa amevalia mavazi rasmi ya chama, Sumaye ameeleza kuwa ameamua kurejea CCM ili apate sehemu ya kutoa ushauri wake kutokana na uzoefu wake katika utawala na siasa.
Ameeleza kuwa yeye hajafikia hadhi ya kudharauriwa kiasi cha kutoa ushauri wake barabarani, hivyo angependa apate mahala pazuri pa kutoa ushauri wake kwa maslahi ya Taifa.
“Nimekuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 na kiongozi kwa miaka kadhaa, nitakuwa sitendi haki kama nitakaa mahali bila kutoa ushauri au mchango wangu kwenye Taifa,” Sumaye anakaririwa.
“Huwezi kutoa mchango kama hauna mahali na ukiutoa barabarani watu watakushambulia, nikaona mimi sio wa hadhi ya kufikia kudharauliwa. Nikasema ngoja nirudi kwenye chama changu kilichonilea, kunikuza na hata kufikia hatua nina mchango wangu kwenye nchi hii,” aliongeza.
Desemba 2019, Sumaye ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alitangaza kuondoka ndani ya chama hicho, ikiwa ni siku kadhaa baada ya kupigiwa kura 48 za hapana kati ya kura 76, hivyo kusababisha uchaguzi wa Uenyekiti wa Kanda ya Pwani kurudiwa. Sumaye alikuwa mgombea pekee.
Alijiuna na Chadema akitokea CCM, Agosti 2015 akifuata nyayo za Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa baada ya wawili hao kutopata nafasi ya kugombea urais kupitia CCM. Sumaye alimpigia kampeni Lowassa akiunga na vyama vingine vilivyounda Ukawa. Vivyo hivyo, Lowassa alirejea CCM Machi Mosi, 2019.