Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, amesema kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally ajiandae kuchukiwa ndani ya chama chake kutokana na kauli zake.
Sumaye amedai kuwa kauli ya Dkt. Bashiru aliyoitoa alipokuwa katika Kongamano la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata), kuwa vitendo vya rushwa na kutowajibika ndivyo vilivyofanya nchi kupata Serikali iliyokosa uhalali wa kisiasa mwaka 2010 baada ya wananchi ambao ni chini ya nusu ya waliojiandikisha kujitokeza kupiga kura, ni kauli ambayo itamuingiza matatani.
“Katika mikutano yangu mbalimbali na wanahabari niliwahi kusema kura ambazo CCM ilipata kwenye uchaguzi wa 2010, chama hiki hakikuwa na uhalali wa kuwa chama tawala tena. Matokeo yake nikaanza kuchukiwa na kutopendwa ndani ya chama,” Sumaye anakaririwa na Mwananchi.
“Hii ndiyo dalili kubwa ninayoiona kwa Dkt Bashiru ndani ya chama chake. CCM hawapendi kuambiwa ukweli kwa sababu watashindwa katika utekelezaji wa majukumu yao mbalimbali,” Sumaye ameendelea kukaririwa.
Sumaye amedai kuwa endapo kauli hiyo wangeitoa wapinzani, wangeweza kuingia matatani kwa kuitwa wachochezi.
Dkt. Bashiru alieleza kuwa vitendo vya rushwa na udanganyifu vilisababisha watu kuona kama chaguzi ni maigizo na vituko, hivyo kujitokeza kwa idadi ndogo ya wapiga kura.