Kiungo Mzawa Salum Abbubakari ‘Sure Boy’ huenda akawa sehemu ya kikosi cha Young Africans kitakachoikabili Simba SC Jumapili (Oktoba 23), kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Young Africans inayoshikilia taji la Ligi Kuu itakua mwenyeji wa mchezo huo uliopangwa kuanza mishale ya saa kumi na moja jioni, huku ikijivunia kumbukumbu nzuri ya kuifunga Simba SC mara mbili mfululizo kwenye michezo ya Ngao ya Jamii na Nusu Fainali Kombe la Shirikiko msimu uliopita.
‘Sure Boy’ aliukosa mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mabingwa wa Sudan Al Hilal uliopigwa mjini Khartoum, ambapo Young Africans ilikubali kufungwa 1-0, kutokana na kutokua ‘FIT’.
Taarifa kutoka Young Africans zinaeleza kuwa Kiungo huyo aliyesajiliwa klabuni hapo mwanzoni mwa mwaka huu akitokea Azam FC amepona Malaria na tupo ‘FIT’ kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba SC.
Taarifa hizo zimeongeza kuwa ‘Sure Boy’ alikuwa sehemu ya wachezaji waliongia kambini Jumatatu (Oktoba 17) kwa ajili ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba SC.
Young Africans inakwenda kukutana na Simba SC ikiwa nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 13 sawa na Simba SC iliyo kileleni, lakini miamba hiyo imetofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.