Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Sven Vandenbroeck, amesema wanatarajia kuanza msimu mpya wa ligi kwa ushindi kama ilivyokuwa katika mchezo wa ufunguzi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Namungo FC mjinji Arusha.
Mabingwa hao watetezi wanatarajiwa kuanza kutetea taji lao mwishoni mwa juma hili kwa kupambana na timu mpya iliyopanda daraja ya Ihefu FC kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Kocha Sven amesema hakuna mchezo rahisi kwenye Ligi Kuu kwa sababu ya ubora wa vikosi vilivyosajiliwa, na kila timu inajipanga kufanya vizuri kwenye michezo ya awali.
Sven amesema wanaamini timu itakayopata ushindi katika michezo ya kwanza, ndiyo itajiweka kwenye mazingira mazuri kwenye mbio za ubingwa na wachezaji wake watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupambana.
“Tuko tayari, tunajua hakuna mchezo rahisi mbele yetu, sisi ndio mabingwa wa msimu uliopita, tunatakiwa kuendeleza ubora wetu, tunahitaji kujiimarisha kila siku,” amesema Sven.
Kikosi cha Simba kiliwasili jijini Mbeya jana Jumanne, kikitokea jijini Arusha kupitia Dar es salaam, na jioni walifanya mazoezi mepesi huku leo asubuhi walitarajiwa kuanza programu maalumu kuelekea mchezo dhidi ya Ihefu.
Simba itashuka uwanjani Jumapili ikiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao sita kwa sifuri walioupata kwenye tamasha la Simba Day dhidi ya Vital’O kutoka Burundi, huku pia ikichukua Ngao ya Jamii baada ya kuwafunga Namungo FC magoli 2-0 Jumapili iliyopita jijini, Arusha.