Kocha wa Mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC, Sven Vandenbroeck amekipongeza kikosi chake kwa kuonyesha soka safi dhidi ya Gwambina FC, na kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri.
Simba SC ilivuna ushindi huo juzi Jumamosi, Septemba 26 Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam na kufikisha alama 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wakitanguliwa na Azam FC wenye alama 12.
Kocha huyo amesema haikua rahisi kwa kikosi chake kufikia lengo la ushindi huo, kutokana na wapinzani wao kuwa imara wakati wote, lakini umahiri na kufuata maelekezo kwa wachezaji wake kulifanikisha lengo la kuibuka na alama tatu muhimu.
“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kufanya vizuri kazi yao wanayopaswa kutimiza, wamepambana, wametengeneza nafasi na kupata ushindi, kwa ujumla nimeridhishwa na kiwango walichoonesha kwenye michezo miwili nikianza na Biashara tulioshinda mabao manne kwa sifuri.” Amesema Sven.
Hata hivyo kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji amesema, kikosi chake kitaendelea na kasi ya mapambano dhidi ya JKT Tanzania kwenye mchezo unaofuata mwishoni mwa juma hili.
Simba SC itakua ugenini kwenye mchezo huo, baada ya kuvuna alama sita kwenye uwanja wake wa nyumbani wakizifunga Gwambina FC na Biashara United Mara.