Beki wa pembeni wa mabingwa wa soka Tanzania bara Simba SC Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, ametaja sababu za kushindwa kuiadhibu ipasavyo Gwambina FC, kwenye mchezo wa mzunguuko wanne wa Ligi Kuu uliochezwa Jumamosi, Septemba 26 Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Simba ilitarajiwa kuibuka na ushindi mkubwa zaidi ya ule walioupata dhidi ya Biashara United Mara, lakini mambo yalikua tofauti na kujikuta wakiambulia alama tatu zilizotokana na mabao matatu.

Beki huyo wa kushoto amesema Gwambina FC walicheza mchezo huo kwa kujihami zaidi, na kutoa nafasi finyu kwa kikosi cha Simba kufikia lengo la kuibuka na ushindi mnene.

“Nawapongeza sana Gwambina FC, walikuja na ‘Mpango’  wao wa kutuzuia na hiyo imewasaidia sana, vinginevyo ingekuwa zahma, lakini wakatupa wakati mgumu mpaka tukabadilisha mbinu na hata kipindi cha kwanza kilipoisha tukaingia vyumbani, kocha alituambia jinsi gani ya kucheza na timu kama hii ‘inayopaki basi’, ndiyo hivyo ukaona tukabadilika na kushinda.” Amesema Tshabalala.

Nahodha huyo msaidizi, amesema  wanachotaka si tu kwamba kila anayekuja Uwanja wa Benjamini Mkapa anafungwa, bali nia yao kubwa ni kuutetea tena ubingwa wao kwa msimu wa nne mfululizo.

Kwa ushindi huo, Simba SC inakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 10 na mabao 10.

Simba SC itarejea dimbani mwishoni mwa juma hili kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kuivaa JKT Tanzania.

JPM alaani mauaji ya kada wa CCM Njombe
Young Africans SC yalaani vurugu

Comments

comments