Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeridhia kutungwa kwa Sheria ya kulinda taarifa binafsi katika mitandao ya simu.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema muswada huo utasomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Bunge utakaoanza Septemba 13, 2022 jijini Dodoma.
Nape ameyasema hayo Septemba 7, 2022, wakati akifungua mkutano wa wadau wa mawasiliano na TEHAMA (Connect to Connect) Afrika.
“Tumekuwa tukisubiri kwa muda mrefu kuwa na sheria ya kulinda data binafsi na habari njema ni kwamba kwa sasa tumeruhusiwa kuendelea na mchakato na mwezi huu sheria itasomwa bungeni,” amesema.
Katika hatua hiyo serikali pia imewataka wadau kutoa maoni ili kusaidia mchakato wa utungwaji wa sheria hiyo.
Mwaka 2021 wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iliahidi kupeleka Bungeni muswada utakaowezesha kutungwa kwa Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi ili kulinda faragha na taarifa za mwananchi.
Wizara pia ilisema imeandaa sheria hiyo ili kulinda faragha na taarifa binafsi za wananchi katika hatua ya ukusanyaji wa taarifa, usafirishaji, matumizi na utunzaji wa taarifa hizo kwa kuwa taasisi mbalimbali zinatumia taarifa husika.