Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amepokea taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika maeneo yote nchini.
Dkt. Samia amepokea taarifa hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Shelui Mkoani Singida, ambapo katika hotuba yake alisema asilimia 90 ya vijiji vyote nchini vimepata umeme na hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliyoelekeza kupeleka umeme katika vijiji vyote nchini kabla ya mwaka 2025.
Aidha alisema kuwa Serikali inafanya juhudi na mipango ya muda mfupi na mrefu kuimarisha umeme wa Gridi ya Taifa ili kuondokana na kero ya kukatika kwa umeme mara kwa mara na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema kwa Serikali ilitoa shilingi Trilioni 1.57 ili kumaliza uunganishaji wa umeme katika Vijiji 4071 ambavyo vilikuwa havina Umeme kabla mwaka 2025 na kulikuwa na Vijiji vingi kuliko awamu zote zilizotangulia.
Akizungumzia agizo lililotolewa Rais, mwezi mmoja uliopita la kutokatika Umeme kwa kipindi cha Miezi 6, Kapinga amesema kuwa, tayari wameimarisha mitambo ya Umeme iliyokuwa imepata hitilafu na kushindwa kuzalisha umeme ya Ubungo I na Tegeta ambayo mpaka sasa imeweza kuzalisha jumla ya Megawati 17.
Kuhusu Mradi wa Julius Nyerere, (JNHPP), Kapinga amesema mpaka sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 92.7 ya utekelezaji wake na kazi inaendelea vizuri ili ifikapo Januari 2024 waanze majaribio ya kuzalisha umeme katika bwawa hilo.