Wananchi wamehimizwa kuongeza bidii kwa kujihusisha na kilimo mseto chenye mazao ya miti, hali itakayosaidia kuepukana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kutunza mazingira na kujipatia kipato kupitia uvunaji mazao na hewa ukaa.
Hamasa hiyo imetolewa na Waziri ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selema Jaffo akiwa wilaya ya Muleba, mkoani Kagera wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi wa biashara ya hewa ukaa awamu ya pili unaotekelezwa na taasisis ya KADERES kupitia ufadhili wa ushirika wa benki ya wakulima ya nchini Uholanzi, RaboBank.
Amesema, “kupitia kilimo mseto ambacho kitahusisha mazao ya miti kama kahawa, miparachichi, karafuu, maembe na korosho mkulima atanufaika mara mbili kwa kuvuna mazao yake na kuuza lakini pia kwa biashara ya hewa ukaa.”
Ameongeza kuwa, “hadi sasa makampuni zaidi ya 20 yamekwishasajiliwa hapa nchini kwa ajili ya kufanya biashara ya hewa ukaa kuanzia mwaka huu”.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima amesema kuwa “zaidi ya wananchi laki mbili watanufaika na biashara ya hewa ukaa kwa kipindi kisichopungua miaka 20.”
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya KADERES inayotekeleza mradi huo, Leonard Kachebonao amesema kuwa wana lengo la kufikia wakulima milioni 10 hapa nchini katika kipindi cha miaka 5 ijayo na kuiomba serikali kuwasaidia ili kutimiza lengo hilo.
Awali, Dausoni Buyeza Mkulima kutoka Karagwe na Rejina Nestory mkulima kutoka Muleba ni miongoni mwa wanufaika wa mradi huo awamu ya kwanza, wamewahimiza wakulima wengine kujihusisha na kilimo mseto kwani kimekuwa na faida kwao pia wamesema kuwa fedha walizopata ziliwasaidia kupata mahitaji ya familia ikiwemo kumudu gharama za elimu kwa watoto wao.