Meneja wa klabu ya Everton Ronald Koeman amesikitishwa na kitendo cha mshambuliaji wake Wayne Rooney, cha kukamatwa na polisi anaendesha gari akiwa amelewa.
Rooney alikamatwa muda mfupi baada ya saa nne usiku kwa saa za Uingereza, baada ya polisi wa Cheshire kusimamisha gari lake aina ya VW Beetle eneo la Wilmslow.
Koeman amesema taarifa hizo zilimsikitisha alipoziona na kuzisikia kupitia vyomvo vya habari, kwani aliamini Rooney alipaswa kuwa kigezo chema kwa wachezaji wengine klabuni hapo, pamoja na vijana chipukizi wa Everton.
Meneja huyo kutoka nchini Uholanzi amesisitiza, kumchukulia hatua za kinidhamu Rooney, ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine kikosini mwake.
“Tulizungumza Jumanne na mwenyekiti Bill Kenwright amezungumza naye kuhusu hali yake,” Koeman amesema.
“Atachukuliwa hatua kwa kufuata utaratibu wa klabu wakati utakapowadia.”
Rooney ambaye ni nahodha wa zamani wa England aliachiliwa kwa dhamana, na anatarajiwa kufika katika mahakama ya hakimu ya Stockport baadae mwezi huu.
Kesi yake kimepangiwa kusikilizwa Septemba 18, siku moja baada ya Everton kukabiliana na Manchester United katika ligi ya nchini England.
Mchezo huo utakuwa ya kwanza kwa Rooney kurejea Old Trafford tangu aliposajiliwa na klabu yake ya utotoni (Everton FC), ambayo aliihama mwaka 2002 na kujiunga na Man Utd.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31, alitangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa ya England mwezi Agosti, na bado anaendelea kuwa mfungaji mabao mengi zaidi katika historia ya timu ya taifa.