Kocha Mkuu wa Tabora United, Mserbia Goran Kopunovic amewakata wachezaji wa timu hiyo kuongeza umakini zaidi na kuepuka makosa yanayoweza kuwagharimu wakati kikosi hicho kitakapo pambana na Ihefu kesho Ijumaa (Desemba 08) katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Highlands Estate, Mbeya unazikutanisha timu zote ambazo hazijashinda mechi zao zilizopita ambapo Ihefu FC ililazimishwa suluhu na Tanzania Prisons huku Tabora ikifungana bao 1-1 na Mashujaa FC.
“Tumekuwa na siku chache za kurekebisha kasoro ndogondogo zilizojitokeza katika mchezo wetu wa mwisho, niwashukuru wachezaji wameonyesha kuguswa, hivyo kuniahidi kupambana zaidi kadri ya uwezo wao ili tupate matokeo mazuri,” amesema.
Goran aliongeza kupata pointi moja ugenini dhidi ya Mashujaa sio jambo baya kwao ingawa anahitaji kuona mabadiliko ya kiuchezaji kwa wachezaji wa kikosi hicho hasa katika utumiaji wa nafasi vizuri kwenye kufunga na katika kuzuia pia.
“Tunatambua wapinzani wetu hawako kwenye wakati mzuri lakini tunaenda kucheza kwa tahadhari zote kwa sababu michezo hii huwa haitabiriki kirahisi, tunawaheshimu sana ila malengo yetu kwa michezo miwili ugenini ni kupata angalau pointi nne.”
Katika michezo 11 iliyocheza timu hiyo, Tabora United imeshinda 3, sare sita na vipigo 2.