Tume ya nguvu za Atomiki nchini, imetakiwa kuwekeza zaidi katika utafiti ili kupata bunifu nyingi hasa kwenye eneo la Sayansi ya Nyuklia, iliyo na muhimu katika ulimwengu wa sasa wa teknolojia kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, teknolojia na ubunifu, Prof. Maulilio Kipanyula kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, katika siku ya Atomiki kwenye maonesho ya wiki ya ubunifu yaliyofanyika uwanja wa Jamhuri, Jijini Dodoma.
Amesema, “TAEC mna kazi kubwa sana ya kuhakikisha mnafanya tafiti zaidi kwenye eneo la sayansi ya Nyuklia kwani karibia ulimwengu wote sasa umegekia huko na lengo ni kukuza uchumi wa nchi na naamini kupitia maonesho haya wananchi watapata nafasi ya kuijua zaidi tume hii.”
Aidha, Prof. Kipanyula ameongeza kuwa, “Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania ni moja ya taasisi muhimu sana katika taifa letu kwa sababu inagusa sekta nyingi sana ukianzia kwenye sekta Afya mionzi inatumika ,kwenye chakula,mbegu na maeneo mengine mengi hivyo ni muhimu sana kuongeza tafiti na wanachi waelimishwe zaidi kuhusu majukumu ya taasisi hii.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Tume hiyo, Prof. Joseph Msambichaka ameitaka tume ya Atomiki kufanya bunifu nyingi zinazotokana na nyuklia kwani Tume hiyo ina uhitaji wa vifaa vingi na vya kutosha.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya nguvu za Atomiki, Prof. Lazaro Busagala alisema wanatarajia kuwa na uwakilishi mkubwa wa wanawake katika sayansi na teknolojia hasa ya Nyuklia, ambapo hivi sasa wametenga jumla ya Shilingi 2.6 bilioni kwaajili ya kuwasomesha wanafunzi ambao wamefanya vizuri katika shahada zao kupitia mpango mkakati wa Dkt. Samia scholarship, ili kupata wabunifu zaidi.
Maonesho hayo, yameandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kushirikisha Taasisi za Elimu ya Juu, Taasisi za Utafiti na Maendeleo, Vyuo vya Ufundi, Mashirika na Taasisi za Umma, Mashirika na Taasisi binafsi za teknolojia, Wizara mbalimbali na Wabunifu.