Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameitaka Taasisi ya UONGOZI Institute kufanya tafiti za kimkakati zitakazoweza kuibua masuala mbalimbali ya kiuongozi kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.
Waziri Simbachawene amesema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi ya UONGOZI jijini Dar es Salaam, ikiwa ni muendelezo wa kuzungumza na Watumishi kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao na kusema tafiti hizo zinatakiwa ziibue mijadala itakayochagiza dhana ya utawala bora.
Amesema, “tunataka mje na tafiti zitakazosomwa duniani kote ambazo zitaleta ukombozi kwa wananchi wa Bara la Afrika hususan katika masuala ya uongozi mfano kwenye suala la rushwa, kwenye masuala ya uongozi bado kunahitajika tafiti nyingi ambazo zitatoa dira ya kuwaandaa viongozi vijana wenye mtazamo wa kimapinduzi.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete ameihimiza Taasisi hiyo kuendelea kuandaa viongozi wa baadae watakaoweza kuendeleza mazuri yanayofanywa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Kadari Singo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi yake, amesema atatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa ikiwa pamoja na kutoa tafiti zitakazoleta matokeo chanya katika jamiii na taifa kwa ujumla.