Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amewataka wajumbe wanaoshiriki kikao cha Uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya kutumia kikao hicho kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto za mipaka badala ya kushindana.
Ameyasema hayo hii leo tarehe 19 Agosti 2019 wakati wa kufungua kikao cha muendelezo wa Uimarishaji mipaka ya kimataifa baina ya Tanzania na Kenya kinachoendelea jijini Arusha.
Amesema kuwa anafarijika sana kuona utatuzi wa changamoto za mipaka ya kimataifa kati ya Kenya na Tanzania unafanywa na nchi husika bila kushirikisha mataifa ya nje na kusema kuwa hiyo inaonyesha ni jinsi gani nchi hizo zinavyoweza kukaa pamoja kwa kujiamini na kupata ufumbuzi wa masuala yake.
Amewataka wajumbe wa kikao cha nchi hizo mbili kutafuta ufumbuzi wa changamoto za mipaka ya kimataifa kati yao kwa kukubaliana na kuzingatia tamaduni za nchi hizo sambamba na miongozo ya viongozi wa nchi husika.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa wa Arusha amewataka washiriki kudumisha pia mahusiano ya kijamii wakati wa majadiliano yao kwa kuwa wananchi wanaoishi mipakani wana mahusiano mazuri ya kindugu na kusisitiza kuwa hali hiyo itadumisha umoja na mshikamano uliopo kati ya nchi hizo.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mathias Kabundugulu amesema kuwa kikao hicho cha siku tano ni muendelezo wa vikao vya uimarishaji mipaka ya kimataifa katika maeneo mbalimbali ya mipakani ikiwa na lengo la kuondoa changamoto kama ilivyoelekezwa na Umoja wa Afrika (AU).
Kwa mujibu wa Kabundugulu, kikao hicho kitapokea taarifa ya ukaguzi wa kipande cha mpaka cha kilomita 128 kutoka eneo la Ziwa Natron hadi Namanga mkoani Arusha ambapo lengo ni kuimarisha mpaka huo hadi Tarakea mkoani Kilimanjaro na baadaye Jasini mkoani Tanga.
Kwa upande wake Mkuu wa Ujumbe kutoka Kenya, Justa Nkoroi amesema kuwa kikao hicho ni muhimu kwa mustakabali wa nchi za Tanzania na Kenya katika kuangalia changamoto za alama za mipaka ya kimataifa iliyowekwa wakati wa ukoloni na kubainisha kuwa ana imani kikao hicho kitatatua changamoto zilizopo na hatimaye kukamilisha kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa na Umoja wa Afrika mwaka 2022.
Tayari jumla ya Kilomita 172 kutoka ziwa Victoria hadi Loliondo mkoani Arusha zimeimarishwa kwa kuwekewa alama (Pillars) za mipaka kati ya Tanzania na Kenya kwa umbali wa mita zisizozidi mita 100 ili zionekane kwa urahisi na wananchi wanaoendesha shughuli zao katika maeneo ya mipakani.