Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani UNICEF, limesema watoto walio katika Pembe ya Afrika na Ukanda wa Sahel wanaweza kufa kwa idadi kubwa iwapo hawata pata misaada ya kibinadamu kwa haraka, kwani wanakabiliwa na utapiamlo mkali na wapo hatarini kupata magonjwa yaenezwayo na ukosefu wa maji.
Idadi ya watu waliokumbwa na ukame katika nchi za Ethiopia, Kenya na Somalia kutokana na uhaba wa maji salama imeongezeka, kutoka watoto milioni 9.5 mwezi Februari hadi kufikia watoto milioni 16.2 mwezi Julai 2022, hali inayo waweka watoto na familia zao katika hatari kubwa ya kuambukizwa magonjwa kama vile kipindupindu na kuhara.
Taarifa iliyotolewa na UNICEF kutoka New York – Marekani, Darak – Senegal na Nairobi – Kenya, imemnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto Catherine Russell akisema historia inaonesha viwango vya juu vya utapiamlo kwa watoto.
Amesema , “Historia inaonesha wakati viwango vya juu vya utapiamlo mkali kwa watoto vinapochanganyikana na magonjwa hatari ya milipuko kama kipindupindu au kuhara, vifo vya watoto huongezeka sana na kwa kusikitisha. Wakati maji hayapatikani au si salama, hatari kwa watoto huongezeka kwa kasi”.
Zaidi ya watoto milioni 2.8 katika pembe ya Afrika na Ukanda wa Sahel, wanakabiliwa na utapiamlo mkali na wapo katika hatari ya kufa kutokana na magonjwa yanayosababishwa na maji mara 11 zaidi kuliko watoto wanaolishwa vizuri.