Faisary Ahmed – Bukoba.
Jeshi la Polisi Mkoani Kagera, linamshikilia mtu mmoja, mkazi wa mtaa wa Mafumbo uliopo kata ya Kashai Manispaa ya Bukoba, baada ya kuchinja na kuonekana akila nyama mbichi ya mbwa katika dampo.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, wamesema walimkuta mtu huyo tayari ameshamaliza kumchuna mbwa huyo na kumuweka kwenye kiroba, huku miguu na utumbo wa mbwa huyo akiuchoma kwenye moto wa dampo hilo.
Wamesema, “huyu jamaa ni kweli amechinja mbwa na udhibitisho ni kwamba tumeona ngozi yake na kichwa ila amesema anatumia kwa matumizi yake mwenyewe na hatukuweza kumhoji zaidi maana askari kituo cha kati wamefika ikabidi waangalie wakadhibitisha ni mbwa basi akachukuliwa.”
Akizungumzia tukio hilo, mchungaji wa Kanisa la Anglikana, Elisha Bililiza amesema, “katika maeneo yetu ya kanda ya ziwa mbwa hatujamgeuza kitoweo, ni rafiki, mlinzi,tunawasiliana nae kwa maana hiyo sisi hatuna huo utaratibu.”
Diwani wa kata ya Kashai, Ramadhan Kambuga amekana kumfahamu mtu huyo na amekemea kitendo hicho huku akisisitiza wananchi wa kata yake kuwa makini wanapo nunua nyama na kusema, “katika nyama inayotakiwa kuliwa kwasisi wana Bukoba Mbwa hayumo.”
Kwa upande wake Afisa mifugo Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Viviano Msigula amesema, “Mbwa katika jamii yetu ya Kitanzania sio mfugo kwa ajili ya kitoweo ni kwa ajili ya ulinzi, mwingine anafuga kama pambo nyumbani na kwenye orodha ya wanyama wanaoliwa Mbwa hayupo.”
Hili linakuwa si tukio la kwanza kwa kumkamatwa mtu akijihusisha na kitendo cha uchinjaji Mbwa katika kata ya Kashai, kwani mwaka jana (2022), aliwahi kukamatwa kijana mmoja aliyekuwa akijihusisha na vitendo hivyo.