Serikali ya Jamhuri wa Muungano Tanzania imetoa ndege ‘Air Bus’ kwa ajili ya mchezo wa Stars dhidi ya Madagascar, ilikutilia kuweka mkazo wa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.
Stars itakuwa na kibarua dhidi ya Madagascar mchezo utakaopigwa Novemba 14 baada ya kumaliza kucheza na DR Congo keshokutwa Alhamis (Novemba 11), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Katibu mkuu wa Wizara ya utamaduni, sanaa na michezo, Dk Hassan Abas amesema Serikali itatoa ndege kwa ajili ya mchezo huo ikiwa ni mkazo wa kuhakikisha timu inafanya vizuri.
“Labda tu niwaambie Serikali katika kuhakikisha tunasapoti michezo tutatoa ndege ya kwenda na kurudi kwa ajili ya mchezo huo, ndege hiyo itabeba wachezaji na benchi lote la ufundi, viongozi, wadau wa soka na waandishi wa habari kwa lengo la kwenda kuhabarisha watanzania.” amesema Abbas
Naye Katibu mkuu wa TFF, Wilfred Kidao amesema tayari wameshaanza maandalizi ya mchezo wao ujao dhidi ya Madagascar.
“Tayari tumeshaanza maandalizi ya mchezo wetu ujao dhidi ya Madagascar, lengo ni kuhakikisha tunapata ushindi.” amesema Kidao
Stars inaongoza Msimamo wa Kundi J ikiwa na alama 7 sawa na Benin huku nafasi ya tatu ikishikiliwa na DR Congo yenye alama 5 na Madagascar inaburuza mkia kwa kuwa na alama 3.