Mwanasiasa wa Taiwan mwenye msimamo mkali wa kuipinga China, Tsai Ingwen amechaguliwa kuwa Rais wa Taifa hilo kwa muhula wa pili kwenye uchaguzi uliofanyika jana.
Tsai ambaye anatoka chama cha Demokrasia cha DPP amepata asilimia 57.2 ya kura huku mpinzani wake kutoka chama cha kizalendo, Han Kuo-yu akipata asilimia 38.6 ya kura.
Imeelezwa kuwa ushindi wake ni ishara ya kuungwa mkono na wapiga kura kutokana na msimamo wa kuipinga China vikali.
katika hotuba yake baada ya kutangazwa mshindi aliionya China ambayo inachukulia kisiwa cha Taiwan kama sehemu ya miliki yake, kutojaribu kutumia nguvu dhidi ya kisiwa hicho chenye Serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.
Ikumbukwe kuwa, Taiwan imejitengenezea taswira ya aina yake tangu ilipojitenga kutoka china wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1949 lakini hadi sasa haijatangaza uhuru wake rasmi.
Huku Serikali ya China ikidai kisiwa hicho chenye watu milioni 23 ni sehemu ya China na imetishia kutumia nguvu kukirejesha chini ya himaya yake.