Bendera zitapepea nusu mlingoti nchini Taiwan kwa muda wa siku tatu kuanzia leo Jumamosi kuomboleza vifo vya watu 50 waliofariki kutokana na ajali ya treni iliyotokea jana Ijumaa.
Watu hao walifariki wakati treni waliyokuwa wakisafiria ilipogongana na lori Mashariki mwa Taiwan.
Maafisa nchini humo wanasema huenda idadi ya vifo ikaongezeka wakati juhudi za uokozi zikiendelea huku Shirika la reli la Taiwan likiwa limeripoti kuwa treni hiyo ilipoteza njia katika kaunti ya Hualien kulipokuwa na ukarabati wa reli.
Maafisa wameongeza kuwa treni hiyo iliyokuwa na abiria 492 na wafanyakazi wanne, ilikuwa safarini kutokea mji mkuu Taipei kwenda Taitung ilipogonga lori lilikouwa na vifaa vya ukarabati ambalo liliteleza kutoka kwenye kilima na kusababisha ajali hiyo.
Waendesha mashitaka wa Hualien wanatafuta waranti ya kumkamata tena meneja anayesimamia shughuli za ujenzi kwenye eneo hilo baada kuachiwa na mahakama kwa dhamana ya kiasi cha dola 17,516 leo Jumamosi.
Ajali hiyo imesababisha vifo vya watu 50 na majeruhi takriban 150 ambao bado wanapatiwa matibabu.