Mkoa wa manyara unalenga kuwachanja watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa Polio unaosababisha kupooza.

Kampeni hiyo itakayozinduliwa rasmi kuanzia April 28 na kukamilika Mei Mosi mwaka huu inalenga kuwachanja na kuwalinda watoto zaidi ya laki tatu wa umri wa chini ya miaka mitano dhidi ya ulemavu na vifo kutokana na mlipuko wa polio ulioibuka nchi jirani ya Malawi.

Kwa mujibu wa Mganga mkuu mkoa wa Manyara Damas Kayera Mpango huo wa dharura wa chanjo utafanyika kwa kuwekwa matone ya chanjo kwenye midomo ya watoto mkoani kote nyumba hadi nyumba na katika shule za msingi.

Kayera amewaambia waandishi wa habari kuwa watawafikia watoto kwa asilimia 100%, lengo likiwa kuwaweka watoto wote mkoani humo salama.

“Tumelenga kuwafikia watoto 351, 364 walio chini ya miaka mitano na hii ni kuhakikisha kwamba wanazuiwa na ugonjwa huu wa Polio ambao umeonekana kuanza kule Malawi, hivyo tunataka huu ugonjwa hapa mkoani kwetu usiwepo hivyo tunahitaji wananchi wetu wawe na afya bora ili waweze kujiletea maendeleo yao”. Amesema Dkt Kayera.

Mtaalamu wa Epidemiolojia kutoka Wizara ya Afya Dokta Witness Mchwampaka amesema wamejipanga kuzifikia jamii za kifugaji na wawindaji wa Kihadzabe katika kufanikisha chanjo hiyo.

Kwa upande wake mratibu wa chanjo mkoa wa Manyara Suleiman Manoza amesema kwa kila halmashauri wametenga timu maalumu kutumia pikipiki kufikia maeneo magumu kufikika.

Peter Banda: Tumejipanga kutimiza lengo ugenini
Waziri wa Mifugo amsimamisha kazi mkandarasi