Takriban watu 84 wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya mlipuko mkubwa kutokea katika mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown.

Mlipuko huo ulitokea baada ya lori la mafuta lenye urefu wa futi 40 kugongana na gari jingine kwenye makutano yenye shughuli nyingi jijini humo.

Rais Julius Maada Bio amesema “amesikitishwa sana na moto huo mbaya na vifo vya kutisha vya watu”.

Kupitia ukurasa wake wa twitter, ameandika serikali yake itafanya “kila kitu kusaidia familia zilizoathirika”.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, Chumba cha kuhifadhia maiti kinachosimamiwa na serikali kimepokea miili 91 hadi sasa, meneja ameliambia shirika hilo.

Brima Bureh Sesay, mkuu wa Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga la Sierre Leone, aliviambia vyombo vya habari kuwa tukio hilo lilikuwa “ajali mbaya”.

Hata hivyo mji huo wa bandari, ambao ni makazi ya watu zaidi ya milioni moja, umekabiliwa na majanga kadhaa makubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Itakumbukwa, Mwezi Machi, zaidi ya watu 80 walijeruhiwa baada ya moto mkubwa katika mojawapo ya vitongoji duni vya jiji hilo kuwaacha zaidi ya watu 5,000 kuyahama makazi yao.

Na mwaka 2017 zaidi ya watu 1,000 walipoteza maisha baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha maporomoko ya matope yaliyokumba jiji hilo, na kuwaacha karibu watu 3,000 bila makazi.

Mwanamuziki maarufu Brazil Marilia Mendonca afariki dunia
Watu 11 wafariki Dunia kwenye Show ya Travis Scott.